Kununua au kuuza hisa zangu?

Kama unataka kununua hisa ambazo zinauzwa kwenye soko la awali (IPO) kuna mawakala maalum ambao huwa wamepewa wajibu wa kuuza hisa kwenye soko la awali. Mwekezaji anatakiwa kujaza fomu ya maombi na kukabidhi pesa kwa wakala kulingana na idadi ya hisa anazotaka kununua na atapewa stakabadhi pamoja na kikonyo cha fomu yako kama uthibitisho.

Kama mwekezaji anataka kununua hisa kutoka katika soko la pili (DSE), basi itabidi awaone madalali wa soko la hisa. Atawaeleza mahitaji yake. Dalali atatoa ushauri lakini uamuzi ni wake.

Ufuatao ni utaratibu wa kuuza na kununua hisa katika soko la pili (DSE):-

Ununuzi

Mwekezaji anayetaka kununua hisa atafuata taratibu zifuatazo:

  1. Wasiliana na dalali wa soko la hisa na kumweleza kusudio lako la kununua hisa
  2. Jaza fomu maalum za kununua hisa na kulipia hisa unazotaka kununua
  3. Dalali ataweka fedha kwenye akaunti maalum ya benki kwa ajili ya kununua na kuuza hisa za wateja
  4. Dalali ataweka oda yako ya kununua hisa kwenye mfumo wa kompyuta wa soko la hisa akitumia namba maalum ya mteja.
  5. Iwapo bei unayotaka kununulia hisa itafanana na bei ya mwekezaji mwingine anayetaka kuuza, basi atakuwa amekununulia hisa hizo. Mwekezaji atapokea cheti cha kuthibitisha kuwa ni mwekezaji kwenye kampuni hiyo.

Uuzaji

Mwekezaji anayetaka kuuza hisa atafuata taratibu zifuatazo:

  1. Wasiliana na dalali wa soko la hisa na kumweleza kusudio lako la kuuza hisa
  2. Kabidhi hati yako ya umiliki wa hisa kwa dalali
  3. Dalali atahakiki umiliki wa hisa hizo kabla ya kuuza. Kama hisa haziko kwenye hifadhi ya hisa, dalali ataziweka kwenye hifadhi kabla ya kuuza
  4. Dalali ataweka oda yako ya kuuza hisa kwenye mfumo wa kompyuta wa soko la hisa akitumia namba maalum ya mteja. Iwapo bei unayotaka kuuzia hisa itafanana na bei ya mwekezaji mwingine anayetaka kununua, basi atakuwa amekuuzia hisa hizo na mwekezaji atalipwa.
Pia mwekezaji anaweza kununua au kuuza hisa kupitia mfumo wa simu ya mkononi kwa kupiga *150*36# na kisha kufuata maelekezo