Kutoa Hatifungani

Soko la hatifungani ni soko la madeni na linahusika na hatifungani zitolewazo na serikali kuu, kampuni na manispaa. Soko hili husaidia Serikali kuu, Serikali za mitaa na kampuni kukusanya mitaji ya muda mrefu ili kujenga miundombinu ya uwekezaji kulingana na matarajio ya muda mrefu. Hatifungani zikishatolewa zinaweza kuorodheshwa kwenye Masoko ya Mitaji. Kuorodheshwa kwa hatifungani huwawezesha wawekezaji kuuza wanapohitaji fedha zao, pamoja na kujua thamani ya hatifungani zao.

Masharti ya Utoaji wa Hatifungani

Kampuni inayotaka kutoa hatifungani inahitaji kukidhi masharti yafuatayo:

  • Inatakiwa iwe imeshaorodheshwa kwenye soko la hisa;
  • Inabidi itoe hatifungani angalau zenye thamani ya TZS 50 milioni kwenye kundi la hatifungani husika. Mauzo zaidi ya hatifungani kwenye kundi sio lazima yafuate masharti hayo;
  • Ni lazima iwe na historia ya kupata faida miaka miwili kati ya mitatu ya karibuni;
  • Inatakiwa kufikia uwiano unaokubalika wa madeni na isizidi 400% ya rasilimali ya kampuni. Wastani wa fedha zitokanazo na uendeshaji na thamani ya deni zima iwe angalau 40%;
  • Itawasilisha waraka wa matarajio ukiambatana na ripoti ya wahasibu yenye taarifa za miaka mitatu iliyotangulia na ripoti ya Wakaguzi wa mahesabu ya mwaka ulioisha;
  • Iwasilishe mtiririko wa fedha angalau kwa miezi 12.
  • Iwapo mtoaji hatakidhi masharti haya, atatakiwa kumtafuta mdhamini anayetimizamasharti muhimu ya utoaji wa hatifungani kuidhamini kampuni kuwa iwapo itashindwa kutekeleza masharti, mdhamini atalipia hatifungani hiyo.
  • Atatakiwa kuingia mkataba na soko la hisa kwa masharti kama yatakavyobainishwa na soko kwa nia ya kumlinda mwekezaji.

Utaratibu wa Kutoa Hatifungani

Mtoaji wa hatifungani ambaye atakuwa amefikia vigezo vya kuorodhesha hatifungani zake soko la hisa (DSE) ni lazima afuate utaratibu ufuatao:

  • Utayarishaji wa waraka wa matarajio kwa ajili ya kuuza dhatifungani kama inavyotakiwa na Kanuni za utoaji wa hisa na dhamana kwa umma;
  • Mtoaji wa hatifungani anatakiwa kumteua dalali kiongozi atakayepeleka maombi ya kuingia kwenye soko la hisa kwa Baraza la Soko na kuarifu soko kuwa amemteua dalali huyo;
  • Mtoaji wa hatifungani na hisa atapeleka maombi yake Mamlaka (CMSA) na soko la hisa kupitia kwa dalali ili yaidhinishwe na Mamlaka na soko; na
  • Waraka wa matarajio uidhinishwe kwa ajili ya kuanza kuuza hatifungani kwenye soko la awali.

Kampuni inayotaka kuingia kwenye soko la hisa inatakiwa kumteua mshauri mkuu ambaye atashirikiana na wataalamu wengine kuandaa Waraka wa matarajio, kutathminisha kampuni na kuwasilisha nyaraka zote kwa Mamlaka ili kupata kibali cha kuuza hisa na hatifungani.